Sunday, 30 April 2017


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akilakiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Said Mecky Sadick na viongozi wengine wa mkoa huo, mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa wa Kimataifa wa Kilimanjaro KIA, Aprili 30, 2017. Makamu wa Rais anaungana na Rais John Pombe Magugfuli na Waziri Mkuu Majaliwa kwenye kilele cha sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi, zitakazofanyika kitaifa mjini Moshi, Jumatatu. (PICHA NA VPO)
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na viongozi mbalimbali waliofika awanjani hapo kumlaki. Anatarajiwa kuhudhuria sherehe za wafanya kazi, Mei Mosi zitakazofanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro Jumatatu.
MABO1
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “Mabodi” akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wazee wa CCM Kisiwani humo katika Ofisi ya Kitengo cha Uratibu wa CCM Chake Chake Mkoa wa Kusini  Pemba.

NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala” Mabodi” amewasihi Wazee wa Chama hicho kisiwani Pemba kusimamia ipasavyo suala la Maadili kwa vijana ili waishi wakiwa na uzalendo wa kweli wa kukitumikia na kukilinda chama dhidi ya wapinga maendeleo wanaotamani kuking’oa madarakani.
Nasaha hizo amezitoa wakati akizungumza na Baraza la Wazee wa Chama hicho kisiwani humo wakati akihitimisha ziara yake kisiwani humo huko katika Afisi ya kitengo cha Uratibu wa CCM, Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba .
Alisema Wazee ni hazina kubwa kwa chama na taifa kwa ujumla kutokana na busara na nasaha zao kuwa ni muongozo mwa nyenzo za kuongeza ufanisi wa maendeleo ya chama hicho katika nyanja ya kisiasa na kiuchumi.
Dkt. Mabodi aliwambia Wazee hao kwamba endapo wataweka mkakati maalum wa kukaa na vijana wao kuwaeleza historia ya Zanzibar kabla na baada ya mapinduzi nasaha hizo zitawajengea ukomavu na misimamo imara ya uzalendo juu ya CCM.
Pia alisema maendeleo na fursa mbali mbali za kiuchumi zilizopo nchi kwa sasa zimetokana na utumishi mzuri,uadilifu na uzalendo wa viongozi hao wastaafu katika sekta za chama na serikali hivyo bado wana nafasi kubwa ya kutumia ujuzi wao kushauri na kukosoa baadhi ya mambo wanayoona hayaendani na misingi ya Wana ASP waliofanya Mapinduzi ya 1964.
“Katika Sayansi ya kisiasa  Wataalamu wanaamini kwamba hakuna upinzani unaodumu katika maisha ya Serikali Tawala inayoongoza nchi kwa mfumo wa utawala wa bora, Haki, Utu na Usawa kwa wananchi wote.
 Pia Chama chetu hakina uadui na wapinzani siku zote tumekuwa tukiwasihi watushauri na kutukosoa watakavyo juu ya masuala mbali mbali ya kisera na Ilaya ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/ 2020,  lakini wasiharibu  wala kuchafua amani na utulivu  wa nchi yetu kwani wao jukumu lao ni siasa na sio vurugu na migogoro hayo hatuwezi kuyavumilia”, alieleza  Dkt. Mabodi.
Aidha  alitoa agizo kwa viongozi na watendaji wa Chama hicho kufanya utafti wa kitaalamu kwa baadhi ya majimbo ya Pemba ambayo CCM imekuwa  ikiaminishwa kwamba inashindwa kwa kila uchaguzi, jambo ambalo alidai sio sahihi mpaka apate maelezo ya kitaalamu  ili kuhakikisha majimbo yote  ya Pemba yanarudi mikononi mwa chama hicho 2020.
Naibu Katibu Mkuu huyo alitamka  kuwa maandalizi ya kuandika historia mpya ya kisiasa kisiwani Pemba toka kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, yanaanza sasa kutokana na kuwepo kwa  mamia ya wanachama wa CUF wanaotamani kuhamia CCM wakati wowote baada ya Chama chao kukosa muelekeo wa kisiasa na kutawaliwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe.
Alisema kwamba chama hicho kinatambua na kulaani vitendo vya uonevu wanavyofanyiwa wafuasi wa CCM vinavyosadikiwa kutekelezwa na wapinzani kisiwani humo  ambao wanachochewa na viongozi wao,  lakini  serikali kupitia vyombo vya Dola wamekuwa wakithibiti hali hiyo, huku Chama kikitafuta ufumbuzi wa kudumu katika kuthibiti hali hiyo.
“ Wanachama wetu wanapopigwa kuchomewa nyumba, kung’olewa mazao yao, kuharibiwa kwa miundombinu ya barabara na kuchomwa ofisi za umma hatusikii viongozi wa CUF wakikemea vitendo hivyo hali ya kuwa wanaofanyiwa sio raia ama hawana haki ya kuishi Pemba kwa Amani”, alisema CCM itaendelea kufanya siasa za kistaarabu  Zanzibar lakini haitovumilia  vitendo  vya uonevu  wakati yenywe ndiyo iliyoweka serikali madarani na kuvisisitiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutafuta ufumbuzi wa tatizo haraka.
Dkt. Mabodi aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, kwa juhudi zao katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wananchi wote bila ya ubaguzi kwa zaidi ya asilimia 90.
Alisema Pemba kwa sasa imekuwa na miundombinu yote muhimu ambayo zamani walikuwa wakiifuata nje ya kisiwa hicho lakini kwa sasa imeimarishwa na Serikali inayotokana na CCM kama ilivyoahidi kwa wananchi kuwa itatoa huduma hizo.
Nao Wazee hao walisifu juhudi za Naibu Katibu Mkuu huyo kwa kasi yake ya utendaji unaolenga kuongeza uimara na nguvu za CCM Zanzibar ambapo wamemtaka awakumbushe baadhi ya viongozi wengine wafuate nyayo zake.
Hata hivyo walimpongeza Dkt. Shein kwa juhudi zake za kuimarisha Sekta ya Afya na miundombinu ya barabara kisiwani Pemba ambayo ni pamoja na uimarishaji wa Hospitali ya Abdalla Mzee inayotoa huduma za kisasa, ambapo wameahidi kuthamini na kulinda huduma hizo.
tp2
Shamrashamra za ushindi mnono na vikombe kwenye michezo minane kati ya kumi ambayo timu za michezo TPDC ilishiriki katika mashiondano ya Mei Mosi.

tp1
Timu za michezo za TPDC zikiwa na mafuriko ya vikombe vya ushindi zilizoupata kwenye mashindano mbalimbali ya Mei Mosi.


………………………………………………………………………..
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lafanikiwa kubeba vikombe vinanena na medali nne katika michuano ya mashindano ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani-Mei Mosi yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Ushirika Mkoani Kilimanjaro.
Katika mashindano hayo yaliyoanza tarehe 19 hadi 29 Aprili, 2017 yaliyoandaliwa na COTWU(T) yalihusisha mashindano katika michezo ya kuvuta kamba, mbio za marathon, mbio za baiskeli, bao, kalata, draft, mpira wa pete na mpira wa miguu kama sehemu ya maandalizi ya siku ya Mei Mosi.
Akizungumza na vyombo vya habari Mwenyekiti wa Michezo wa TPDC ndugu Nelson Rwechunguraalieleza kuwa timu yake imezidi kuwa bora zaidi kwakuwa mashindano yaliyopita ilifanikiwa kuchukua jumla ya vikombe vitano na medali tatu lakini katika mashindano ya safari TPDC imefanikiwa kuchukua vikombe vinane na medali nne.
“Tumeweza kuchukua kikombe cha mshindi wa wa tatu katika mashindano ya kuvuta kamba kwa wananume, kikombe cha mshindi wa pili katika mashindano ya kuvuta kamba kwa wanawake, kikombe cha mshindi wa tatu katika mbio za baiskeli kwa wanawake na kikombe cha mshindi wa pili kwa upande wa wanaume, kikombe cha mshindi wa pili katika mashindano ya marathon kwa wanaume na kikombe cha mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na kikombe kwa mshindi wa tatu katika mchezo wa draft’’ alieleza  mwenyekiti wa TPDC.
Kwa mujibu wa ndugu Rwechungura wafanyakazi wa TPDC walioipatia timu vikombe ni Diana Byonge na Peter Ngalu kwa upande wa baiskeli, Neema Mdegela na Darush Shija kwa upande wa mbio ndefu na Diana Byonge katikamchezo draft.
Aidha akizungumzia kushindwa kuchukua ubingwa wa mpira wa miguu, Mwenyekiti alieleza kuwa pamoja na kufungwa na timu Geita Gold Mining, kwake yeye timu yake ndiyo bingwa wa mashindano kutokana na mpira mzuri walioonyesha katika mtanange huo pamoja na kuwa pungufu kwa muda mrefu.
“Pamoja na kushindwa kuchukua ubingwa wa mpira wa miguu, bado kwangu mimi naichukulia timu yangu kama ndiye bingwa wa mashindano hayo kwakuwa tumecheza kwa kiwango bora zaidi na hata watazamaji wameshuhudia hilo na hivyo tumepata faraja na pia tunawapongeza Geita kwa ushindi walioupata ingawa changamoto zilikuwepo kwa upande wa maamuzi lakini ndio mchezo na tunatumaini zitafanyiwa kazi katika mashindano yajayo’’ alieleza mwenyekiti.
Kwa upande wake Kapteni wa timu ya mpira wa miguu TPDC ameeleza kuwa hatua waliyofikia ya kuwa washindi wa pili ni ya kumshukuru Mungu kwakuwa timu bora zilikuwa nyingi lakini ‘wao walifanikiwa kufika hatua ya fainali.
“Kiukweli najivunia kuwa na timu bora zaidi kwenye mashindano haya na hiiimedhihirishwa na ushindi tuliokuwa tukiupata hadi kufikia hatua na tumecheza vizuri saana pamoja ya kuwa pungufu kwa zaidi ya dakika 76 lakini bado tumeweza kuwadhibiti wa pinzania wetu kwa muda mrefu hadi walipoweza kutufunga gori la pili ambapo hadi mwisho wa mchezo tulitoka gori mbili kwa moja’’ alichambua kapteni wa TPDC.
Aidha alisisitiza kuwa waajiri wanapaswa kuzingatia na kusisitiza michezo kwa wafanyakazi ili kuboresha afya za wafanyakazi, kuleta umoja na kutangaza shughuli za Mashirika kwa wananchi.


Mheshimiwa Nabii Mkuu Dr GeorDavie Royal Mkuu ,   jana amezindua rasmi kitabu cha " KUKIWA NA FOLENI" kilichoandikwa na Wiseman Luvanda.
Pia Nabii Dr.GeorDavie alimpongeza kwa kitendo chake  alichoamua kufanya kwa kuwa balozi wa barabarani  kwa kutoka Jijini Dar es salaam hadi mkaoni Arusha wa usafiri wa baiskeli
Akizungumza na wadau waliohudhuria hafla hiyo mtunzi wa kitabu hicho alisema vijana wanapaswa kutumia vipaji vyao kwa kujituma, kuthubutu na kufanya kazi kwa nguvu  na si kulalamika kila siku,  jambo linalopelekea kuibuka kwa makundi mbalimbali kama vile Panya Road na mengineyo.
Aidha mwandishi huyo amewataka wadau mbalimbali kumuunga mkono katika kukinunua kitabu hicho cha " KUKIWA NA FOLENI" , ambacho pia amekiandika kwa lugha ya Kiswahili  ili kuweza kukisambaza nchi nzima.
Tazama baadhi ya picha za tukio hili hapo chini

Pichani ni Mwandishi wa kitabu hicho Wiseman Luvanda, Akizungumza na baadhi ya wadau waliohudhuria kongamano hilo jana Jijini Arusha. Picha na msumbanews blog

Nabii Mkuu Dr GeorDavie Royal Mkuu akipokea kitabu kutoka kwa Mwandishi Wiseman Luvanda.Picha na msumbanews blog

Baadhi ya wadau mbali waliojitokeza kwenye kongamano  la kuinuliwa viwango na uzinduzi wa kitabu hicho.Picha na msumbanews blog

Mwandishi Wiseman Luvanda akifuatilia kwa makini kongamano la kuinuliwa viwango ambalo lilifuatana na uzinduzi wa kitabu chake.Picha na msumbanews blog


Na Magreth Subi,Moshi
Shirika la umeme Nchini Tanzania (TANESO) limeibuka kidedea katika maonesho ya wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) ambayo yamefikia kilele chake Aprili 28, 2017 Mjini Moshi.
 Mgeni Rasmi katika maonesho hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama,(pichani katikayi), alitoa pongeza kwa TANESCO kwa Huduma nzuri inayotolewa katika kuhudumia jamii na kuwataka Wafanyakazi kuwa na ari siku zote pamoja na changamoto wanazokutana nazo kwani changamoto ndio chachu ya maendeleo kuelekea Nchi ya Viwanda kama kauli mbiu ya Mhe. Rais inavyo sema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mhagama alitoa shukurani kwa washiriki na kutangaza washindi katika Nyanja mbali mbali na TANESCO kuibuka mshindi wa kwanza wa masuala ya Afya na Usalama kazini mahala pa Kazi katika Sekta ya Huduma kwa Wateja.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu kitengo cha Afya na Usalama Kazini Bw. Fred Kayega alitoa maelezo ya vifaa mbalimbali vya vinavyotumiwa na Wafanyakazi kujikinga na ajali pahala pa kazi kwa Mhe. Mhagama alipotembelea banda la TANESCO kabla maonesho hayo hayajafikia hitimisho.

Baadhi ya Wafanyakazi wa TANESCO Makao Makuu, pamoja na Wafanyakazi wa Mkoani Kilimanjaro, walifurahia ushindi huo kwani utazidi kuongeza hari kwa Wafanyakazi na kufanya vizuri Zaidi katika utendaji wa Kazi.

Mfanyakazi wa TANESCO akitoa maelezo kwa Mhe. Waziri


NA JUMA FARID, ZANZIBAR.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na baadhi ya Jumuiya za wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini zinazoonyesha nia ya kuthamini  fani ya Ujasiriamali kama chanzo mbadala cha kupunguza tatizo la Ajira nchini.
Ahadi hiyo imetolewa na  Mkurugenzi  wa Viwanda Zanzibar, Saleh Suleiman Hamad  kwa Niba ya  Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko  Balozi Amina Salum Ali Wakati akifunga warsha ya Mashindano ya miradi ya Ujasiriamali kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar ( ZU) huko Kampasi Kuu ya Chuo hicho Tunguu.
Amesema ubunifu ulionyeshwa na wanafunzi hao katika uandishi, mikakati na bidhaa  za miradi ya Ujasiriamali waliyoiwasilisha katika Mashindao hayo inajenga ushawishi kwa serikali na mashirika mengine ya kimataifa kuwaunga mkono ili wafikie malengo yao ya kujiajiri na kuwaajiri vijana wengine wasiokuwa na ajira.
Amesema bado wanafunzi wengi wanaohitimu elimu ya ngazi ya vyuo vikuu nchini hawajatumia fursa zinazopatikana katika fani ya Ujasiriamali ambayo imekuwa ikitegemewa na mataifa mbali mbali duniani kupunguza  tatizo la ajira hasa kwa vijana.
“ Nasaha zangu kwenu kabla ya kuanzisha mradi wowote fanyeni tathimini na utafti wa kitaalamu kubaini aina ya ujasiriamali unaotaka kufanya una maslahi gani na wateja wako wahitaji bidhaa za aina gani sambamba na kuwa wabunifu wa kufanya miradi isiyofanana.”, alisema Katibu huyo.
Aidha alieleza kwamba kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali serikali itaendelea kudhamini miradi itakayoonyesha ustawi na maendeleo endelevu.
Pia  katika juhudi za kuwajengea uwezo wajasiriamali hao alieleza kwamba serikali itashawishi makampuni na mashirika ya kimaita ya kibiashara kufanya kazi kwa karibu na jumuiya hizo ili zipate soko la uhakika la kuuzia bidhaa zao.
Hata  hivyo ametoa nasaha zake kwa wajasiriamali hao kutengeneza bidhaa bora zitakazokubalika katika soko la kimataifa pamoja na kujiongeza kitaaluma kupitia mafunzo mbali mbali ya fani hiyo.
Mapema  akizungumza  Mlezi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar(ZU), Bw. Juma Rashid Khamis  ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo hicho aliwasihi washiriki wa mashindao hayo kuendelea kujifunza zaidi kupitia kwa wajasiria mali wakongwe ili wapate ujuzi wa ziada wa kukabiliana na ushindani wa bidhaa na miradi ya ujasiriamali ndani na nje ya Zanzibar.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya SISI Consultants, Mohamed  Wario  aliwataka Wasomi hao kutumia  vizuri  fursa hiyo ya ujasiria mali kwa kuangazia  sehemu tofauti  ambazo bado hazijatumiwa  vizuri  kibiashara  zikiwemo  Sekta ya Utalii, Uvuvi na Ufugaji ili kuzalisha bidhaa bora zinazotokana na rasilimali hizo na kuzishindanisha katika soko la ndani na nje ya nchi.
“ Kampuni  ipo tayari kushirikiana na nyinyi  wakati wowote  lakini lazima mjiongeze zaidi kufikia lengo la kufanya miradi bora na inayoendana na mahitaji ya sasa ili mpate mafanikio zaidi”, alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake mshiriki wa mashindano hayo aliyeshindanisha mradi wa usindikaji wa bidhaa aina ya Jam inayotumia kwa chakula cha mkate iliyotengenezwa kwa matunda ya Maembe, Ehlam Ali Khamis alisema wazo la kutengeza bidhaa hizo ni kutokana na kukosekana kwa matumizi mazuri ya matunda hayo hasa wakati wa msimu wake hali inayosababisha kuharibika kwa kukosekana kwa viwanda vya kusindika matunda hayo.
Akitoa ufafanuzi juu ya  Warsha hiyo,  Mwanzilishi na Msimamizi  wa Mashindano hayo  Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Zanzibar  ZANUSO,  Mohamed Omar  alifafanua kwamba awali mchakato huo ulishirikisha jumla ya vyuo Sita na ulipopita mchujo vikabaki vitatu ambavyo ni Zanzibar University (ZU), State University  of Zanzibar(SUZA) na Summait University.
Mashindano hayo wamepatikana washindi saba ambao wamepewa Zawadi mbali mbali zikiwemo simu za Adroid, lakini nafasi ya kwanza ambayo imeshikiliwa na Issah Eugenio kwa mradi wa Handbags Made in Jeans, nafasi ya pili ni Ehlam Ali Khamis kwa mradi wa Mango Jam na Tatu Ibrahim ahmad abdalla na Sabrina  Khamis Machano wa mradi wa Teke knowlge solutions company  wote kutoka vyuo tofauti vilivyoshiriki kwa awatua hiyo.Mkurugenzi wa Kampuni ya SISI Consultants, Mohamed  Wario ambayo ni miongoni mwa wadhamini akitoa nasaha zake kwa wanafunzi walioshiriki katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na  jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar(ZANUSO) huko ZU kampasi kuu ya Tunguu.


Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Viwanda Zanzibar, Saleh Suleiman Hamad akiutubia wakati wa kufunga mashindano yaliyoandaliwa na  jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar(ZANUSO) huko ZU kampasi kuu ya Tunguu.Picha ya pamoja ya washiriki wa mashindano hayo

Picha ya pamoja ya washiriki wa mashindano hayo pamoja na Viongozi wa ZANUSO na ZU pamoja na mgeni rasmi.